Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu, Utawala na Mipango kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Dkt. Abdul-Nasser Hikmany, amewataka wafanyakazi wa Afisi hiyo kuendelea kushirikiana vyema katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta ufanisi kwa Afisi na Taifa kwa ujumla.
Ametoa wito huo katika ukumbi wa Afisi hiyo wakati akikabidhi majukumu ya kazi kwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Utawala na Mipango, Bi. Fatma Idd ambaye amerejea kutoka masomoni.
Dkt. Abdul-Nasser amesema ushirikiano alioupata kutoka kwa wafanyakazi kipindi chote alichokaimu nafasi hiyo, umempa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayowahusu wafanyakazi, hasa masuala ya kujituma na uwajibikaji kwa kwa maendeleo ya Afisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Utawala na Mipango, Bi. Fatma Idd amemshukuru Kaimu Mkurugenzi huyo kwa uongozi na uwajibikaji wake uliochochea kasi ya maendeleo ya Afisi.
Aidha, amewapongeza wafanyakazi wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha shughuli zote za kazi zinafanyika kwa ufanisi.
Mkurugenzi Fatma amewasisitiza wafanyakazi kuendelea kudumisha maadili ya Utumishi wa Umma ikiwemo nidhamu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utendaji kazi wa Afisi na kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Nao wafanyakazi wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu wameahidi kuendelea kushirikiana, kufanya kazi kwa weledi pamoja na uwajibikaji ili kufanikisha malengo ya Afisi na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Abdul-Nasser Hikmany ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mapitio na Utafiti wa Sheria alikuwa akikaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Rasilimali Watu, Utawala na Mipango kwa takriban mwaka mmoja ambapo Mkurugenzi wa nafasi hiyo alikuwa masomoni.
Matukio
13 Aug 2026
60 views
Wafanyakazi Wahimizwa Ushirikiano katika Kazi
Muhtasari:
Dkt. Abdul-Nasser akabidhi majukumu kwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Utawala na Mipango Bi. Fatma Idd huku wakihimiza ushirikiano kwa wafanyakazi.