Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar - AGCZ

Bendera ya Taifa
Namna Watumishi Wanavyoweza Kupata Fao la Kuumia Kazini kutoka ZSSF
Uandishi wa Sheria

Namna Watumishi Wanavyoweza Kupata Fao la Kuumia Kazini kutoka Zssf

26 Jun 2026 Na Mwandishi Maalum-ZSSF 84 views
Makala hii inaelezea namna ya Watumishi wanavyoweza kupata Fao la kuumia kazini kutoka ZSSF

Hifadhi ya jamii ni dhana pana na kongwe inayotoa ufumbuzi wa matatizo ya kijamii na kiuchumi yanayoikumba jamii.

Hifadhi hiyo ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazomlinda mfanyakazi dhidi ya majanga mbalimbali au kwa upande mwengine inaweza kutafsiriwa kuwa ni mfumo wa kuendeleza kipato cha mfanyakazi pale ambapo kipato hicho kinapungua au kusimama kwa sababu mbali mbali.

Sababu hizo zinaweza kuwa uzee, ulemavu, ugonjwa wa kudumu, kuumia kazini, ukosefu wa ajira na majanga mengine yanayoweza kumpata mfanyakazi.

Kwa mujibu wa Ibara ya 25(1) ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (Universal Declaration of Human Rights, 1948), hifadhi ya jamii ni haki ya msingi ya kila mwananchi duniani.

Aidha, utekelezaji wa tamko hilo uliendelezwa kupitia Azimio la Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu Viwango vya Chini vya Hifadhi ya Jamii, Namba 102 la mwaka 1952, ambapo ibara za 25, 53 na 59 zinaelezea juu ya haki ya wafanyakazi kupata hifadhi ya jamii.

Mbali na matamko na mikataba mbalimbali ya kimataifa, nchi nyingi duniani ikiwemo Zanzibar zimeendelea kuchukua hatua za kutunga sera, sheria na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wafanyakazi wanalindwa dhidi ya majanga mbalimbali, ikiwemo kuumia kazini wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) umejikita katika utoaji wa Mafao mbali mbali, kwa lengo la kumlinda mfanyakazi dhidi ya yanayoweza kumtokezea.

Mfano wa mafao hayo yanayotolewa hadi sasa ni:-

  1. Fao la kuumia Kazini (Employment injury benefit)
  2. Fao la Uzee (Old age benefit)
  3. Fao la Ulemavu wa kudumu (Invalidity benefit)
  4. Fao la Uzazi (Maternity benefit)
  5. Fao la upotevu wa ajira (Unemployment benefit)
  6. Fao la Urithi (Survival benefit)

Fao la Kuumia Kazini

Kwa upande wa Zanzibar, msingi mkuu wa uwepo wa Fao la Kuumia Kazini (employment injury benefit), unatokana na Kifungu cha 10(g) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambacho kinaeleza kuwa ni wajibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, na msaada unatolewa kwa wasiokuwa na uwezo, wazee, wagonjwa, watoto na watu wenye ulemavu.

Aidha, msingi mwingine wa kisheria wa malipo ya Fao la Kuumia Kazini ni Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, Namba 2 ya mwaka 2005, ambayo kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 5 ya mwaka 2022 iliongeza Fao la Kuumia Kazini kuwa miongoni mwa mafao sita yanayotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na utaratibu endelevu na wenye ufanisi wa kulipa fao hili, Serikali kupitia ZSSF ilitunga Kanuni ya Fao la Kuumia Kazini ya mwaka 2023. Fao hili lilianza rasmi kulipwa tarehe 01 Julai 2023 kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi walioumia kazini.

Vigezo vya Kustahili Fao la Kuumia Kazini

Fao la Kuumia Kazini hulipwa kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi ambao ni wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF). Vigezo muhimu vinavyozingatiwa katika kulipa fao hili ni pamoja na:

  1. Mfanyakazi kuumia akiwa kazini;
  2. Mfanyakazi kufariki kutokana na ajali au mazingira ya kazi; na
  3. Mfanyakazi kupata maradhi yatokanayo na kazi (Occupational Diseases).

Aina za Mafao ya Kuumia Kazini

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar hulipa mafao yafuatayo chini ya Fao la Kuumia Kazini:

  1. Fao la Maumivu ya Muda;
  2. Fao la Ulemavu wa Kudumu usiomzuia mfanyakazi kurejea kazini;
  3. Fao la Ulemavu wa Kudumu unaomzuia mfanyakazi kurejea kazini;
  4. Fao kwa mtu anayemhudumia mgonjwa asiyejiweza; na
  5. Fao la Kifo.

1. Fao la Maumivu ya Muda

Fao hili hulipwa kwa mfanyakazi aliyepata maumivu kutokana na ajali au maradhi yatokanayo na kazi wakati au katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi.

Fao hili hukokotolewa kwa kuzingatia kiwango cha maumivu aliyopata mfanyakazi baada ya ajali au maradhi yanayotokana na kazi.

Kiwango cha fao ni sawa na nusu ya pato la siku la mfanyakazi likizidishwa kwa idadi ya siku ambazo mfanyakazi hakuhudhuria kazini kutokana na maumivu hayo.

Hata hivyo, fao hili halitalipwa iwapo mfanyakazi atakuwa amepewa muda wa mapumziko usiozidi siku tatu (3).

2. Fao la Ulemavu wa Kudumu Usiozuia Kurudi Kazini

Fao hili hulipwa kwa mfanyakazi aliyepata ajali au maradhi yatokanayo na kazi yaliyosababisha ulemavu wa kudumu lakini ambao haukumzuia kurejea kazini.

Fao hili hukokotolewa kwa kuzingatia asilimia ya ulemavu aliyopata mfanyakazi ikizidishwa na mshahara wa kima cha chini wa miezi 48.

3. Fao la Ulemavu wa kudumu unaomzuia kurudi kazini

Fao hili hulipwa kwa mfanyakazi aliyepata ajali au maradhi yatokanayo na kazi yaliyosababisha ulemavu wa kudumu ambao unamzuia kurejea kazini tena.

Fao hili hukokotolewa kwa kuzingatia asilimia ya ulemavu husika kwa msingi wa mshahara wa miezi 48.

4. Fao kwa mtu mgonjwa anayemhudumia asiyejiweza

Fao hili hulipwa kwa mtu wa karibu au mtu mwingine yeyote anayemhudumia mfanyakazi aliyepata ulemavu wa kudumu na ambaye hawezi kujihudumia kutokana na ajali au maradhi yatokanayo na kazi. Kiwango cha fao hili ni robo ya kiwango cha fao la ulemavu wa kudumu alicholipwa mfanyakazi husika, na hulipwa kwa mkupuo mmoja.

5. Fao la Kifo

Fao la kifo hulipwa kwa wategemezi wa mfanyakazi aliyefariki akiwa kazini au kutokana na ajali au maradhi yatokanayo na kazi.

Fao hili hulipwa mara moja kwa mkupuo sawa na mshahara wa miezi 48 wa mfanyakazi aliyefariki.

Fao la kifo ni sehemu ya mali ya marehemu na hulipwa kwa warithi wake kupitia:

• Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar kwa mfanyakazi Muislamu; au
• Wakala wa Usajili wa Mali na Biashara Zanzibar kwa mfanyakazi asiye Muislamu.

Utaratibu wa kuomba fao la kuumia kazini

Maombi ya fao la kuumia kazini yanaweza kufanywa na mfanyakazi mwenyewe au mtu mwingine kwa niaba yake kwa kumuandikia Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF ndani ya kipindi cha wiki 12 tangu kutokea kwa ajali, kifo au kugundulika kwa maradhi yatokanayo na kazi.

Maombi hayo huwasilishwa kwa kujaza Fomu ya Maombi ya Fao (SSF 18) pamoja na kuambatisha nyaraka zifuatazo:

  1. Nakala ya kadi ya uanachama wa ZSSF;
  2. Cheti cha kifo (kwa madai ya kifo);
  3. Taarifa ya daktari au matibabu;
  4. Hati ya Polisi (PF3 au PF90);
  5. Slipu ya mshahara;
  6. “Sick sheet” au karatasi ya mapumziko ya matibabu;
  7. Taarifa nyingine yoyote itakayohitajika; na
  8. Taarifa ya Bodi ya Madaktari kwa mfanyakazi aliyepata ulemavu wa kudumu unaomzuia kurejea kazini.

Maombi hayatapokelewa wala kuzingatiwa iwapo yatawasilishwa nje ya muda wa wiki 12 tangu kutokea kwa tukio husika.

Muda wa kulipa mafao

Malipo ya fao la kuumia kazini hulipwa ndani ya siku 14 hadi 28 kulingana na aina ya maumivu au ukamilifu wa vielelezo vya madai viliyowasilishwa.

Mfumo wa malipo ya fao la kuumia kazini

Malipo ya fao la kuumia kazini hufanywa kwa njia ya mkupuo mara moja tu, kulingana na maelekezo ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.

Fao la kuumia kazini ni miongoni mwa mafao muhimu yanayotolewa na ZSSF kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya madhara yatokanayo na kazi.

Uwepo wa fao hili unaonesha dhamira ya Serikali Zanzibar katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanapata hifadhi ya kijamii wanapopatwa na majanga yanayotokana na kazi.

Ni muhimu kwa waajiri na wafanyakazi kuelewa haki, wajibu na taratibu zinazohusiana na fao hili ili kuhakikisha wafanyakazi kuwa wanaostahili wanapata huduma hiyo kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.

Usikose Makala itakayozungumzia Mafao Mengine, utaratibu wa kupata Mafao hayo na nani anastahili kupata mafao hayo.

Kiambatanisho

Unaweza kufungua au kupakua nyaraka inayohusiana na makala hii.

Kuhusu Mwangaza wa Sheria

Mwangaza wa Sheria ni sehemu ya elimu kwa umma inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria, haki, wajibu na taratibu mbalimbali za kisheria.

Makala Zinazohusiana

Hakuna makala zinazohusiana kwa sasa.