Historia ya utungaji sheria Zanzibar ilianza tangu Sultan wa Oman alipoanzisha utawala wake Zanzibar hapa mnamo 1832, ambapo Zanzibar ilikuwa Makao Makuu ya Utawala huo.
Sheria za Kiislam zilikuwa sheria za msingi za Zanzibar na mahkama zilianzishwa na kusimamiwa na Sultan mwenyewe. Sultan alitoa haki kwa Mabalozi wa Nchi za Nje kusimamia raia wa nchi zao.
Uingereza ilitumia Mamlaka ya ziada kwa kuanzisha Ubalozi uliokuwa na uwezo wa kushughulikia kesi za madai na jinai baina ya raia wa Kiengereza na malalamiko yaliyoletwa na raia wa Sultani dhidi ya raia wa Kiengereza na utaratibu huo uliendelea hadi 1861.
Mnamo Juni 14 mwaka 1890, Zanzibar ilikuwa Himaya ya Kiengereza na Waziri wa Kwanza wa Sultani wa Zanzibar akateuliwa kuwa Mwakilishi wa Uingereza.
Mwakilishi huyo alikuwa na dhamana ya Posta, Ofisi ya Kazi, Forodha, Bandari, hazina na Polisi. Madaraka ya Sultani yalikuwa yamepunguzwa na hakuwa na uwezo wa kumuondoa au kumuhamisha Afisa wa Kiengereza na hata mshahara wake ulipangwa na Mamlaka ya Uingereza.
Zanzibar Order in Council 1897
Amri hii ilikuja kuhalalisha kutumika kwa Sheria za India na Uingereza. Kwa Amri hii, sheria zifuatazo zilitumika Zanzibar:
Indian Lunacy Act;
Indian Penal Code;
The Whipping Act;
Indian Succession Act;
Indian Divorce of Marriage;
Bombay Civil Court Act;
Indian Evidence Act; na
Indian Limitation Act;
Zanzibar Council Protectorate
Baraza hili lilianzishwa Aprili 21 mwaka 1925 na lilikuwa Baraza la Kumshauri Sultan likiwa na wajumbe wafuatao na halikuwa na Muafrika hata mmoja:
Sultani - Mwenyekiti;
British Resident - Makamu Mwenyekiti,
Mwanasheria Mkuu,
Katibu Mkuu Kiongozi,
Katibu wa Masuala ya Fedha na,
wajumbe wengine watatu wa kuteuliwa.
Order in Council 1926
Amri hii iliwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Kutunga Sheria na Baraza la Utawala. Kuundwa kwa vyombo hivi viwili kuliweka utawala wa Serikali ya Zanzibar mikononi mwa British Resident na kutaka kwamba Sultani asitunge sheria bila ushauri na ridhaa ya Baraza la Kutunga Sheria.
Order in Council 1936
Amri hii iliruhusu watu wa Zanzibar, kwa baadhi ya kesi kuomba rufaa British Court of Appeal for Eastern Africa.
Baraza la mwanzo la Kutunga Sheria liliundwa likiwa na maafisa 8 na wajumbe 7 wasio maafisa na likiongozwa na Rais wa Baraza hilo.
Kati ya Wajumbe hao 7 kulikuwa na Waarabu 3, Wahindi 2, Muingereza 1 na Muafrika 1. Muafrika wa mwanzo kuwemo katika Baraza hilo alikuwa Sheikh Ameir Tajo ambaye alibaki katika Baraza hilo hadi Mapinduzi ya mwaka 1964.
Utungaji Sheria Baada ya Mapinduzi
Baraza la Mapinduzi (The Zanzibar Revolutionary Council).
Mara baada ya Mapinduzi 1964, Amri ya mwanzo kupitishwa ni Sheria ya Mamlaka ya Kutunga Sheria (Legislative Powers Law) 1964, ambayo iliunda Baraza la Mapinduzi na kulipa uwezo wa kutunga Sheria. Kifungu cha 2 cha Sheria hiyo kilieleza kama ifuatavyo:
“2. The power to make laws for the Government of the Peoples’ Republic of Zanzibar is hereby vested in the President of the Republic acting by and with the advice and Consent of the Revolutionary Council”.
Sheria iliyofuata baadae ni Existing Law Decree No. 1/1964, ambayo ilikuja kuhalalisha kutumika kwa sheria za kabla ya Mapinduzi kwa sharti kwamba zisomwe na mabadiliko muhimu ya kimapinduzi ili ziwiane na hadhi ya Jamhuri.
Pamoja na kuruhusu Sheria za nyuma kutumika, Katiba ya Zanzibar ya 1963 ilipigwa marufuku kutumika. Kuanzia hapo Mamlaka ya Kutunga Sheria yalikuwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Sheria hizi kama zile tulizozipokea kutoka nje zinaitwa “Decrees”.
Mnamo Aprili 26 mwaka 1964, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kupatikana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baadhi ya Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yalianza kushughulikiwa kimuungano chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo, baadhi ya sheria zilizokuwa zinatumika Zanzibar ziliathiriwa na muungano. Mambo hayo yameorodheshwa katika Jedweli la Kwanza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977.
Baraza la Kwanza la Wawakilishi la Zanzibar
Mnamo Oktoba 1979, Baraza la Mapinduzi lilipitisha Katiba ya Zanzibar ya 1979 ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar likiwa na wajumbe 109. Kifungu cha 22 cha Katiba ya Zanzibar ya 1979 inasomeka kama ifuatavyoi:
“22(1) Bila kuathiri masharti mengine yaliyomo katika ibara hii, Baraza la Wawakilishi litakuwa na wajumbe wafuatao:
Wajumbe wote wa Baraza la Mapinduzi isipokuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Wabunge wote wa kuchaguliwa na Wilaya za Uchaguzi waliomo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka Tanzania Visiwani;
Wajumbe wawili wa kuchaguliwa kutoka kila Kamati ya Mapinduzi ya Wilaya waliochaguliwa na Kamati ya Mapinduzi ya Wilaya.
Wajumbe wawili wa kuchaguliwa kutoka kila Kamati ya Mapinduzi ya Mkoa waliochaguliwa na Kamati ya Mapinduzi ya Mkoa;
Makatibu wote wa Mikoa ya Tanzania Visiwani kwa mujibu wa madaraka yao;
Wajumbe wawili wa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya Mkoa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa kila Mkoa;
Wajumbe wawili wa Tanzania Visiwani kutoka katika kila Jumuiya inayoongozwa na Chama waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi;
Wajumbe wasiozidi kumi walioteuliwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar.”
Baraza la Wawakilishi kwa Mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984
Katiba ya Zanzibar ya 1979 ilifutwa na kuazishwa kutunga Katiba mpya ya mwaka 1984. Pamoja na mambo mengine, Katiba hiyo ilibadilisha Muundo wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe wake walikuwa kama ifuatavyo;
Wawakilishi wa kuteuliwa majimboni;
Wawakilishi 10 wa kuteuliwa na Rais.
Wajumbe wanawake wa kuteuliwa;
Wakuu wa mikoa, na
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Muundo huo ulikuja kurekebishwa na Marekebisho ya 2010 ya Katiba ya Zanzibar kwa kuwaondoa Wakuu wa Mikoa, kuongeza idadi ya Wawakilishi wanawake kutoka ailimia 30 hadi 40 na kumfanya Spika mjumbe pale ambapo hakutokana na wajumbe wa kuchaguliwa.