Uchaguzi si jambo geni katika nchi yoyote ya kidemokrasia. Ni jambo la kushirikisha Wananchi katika kuendesha nchi yao, kinyume na nchi zinazofuata mifumo ya kidikteta au kifalme.
Uchaguzi ni mfumo ulioletwa na Azimio la Haki za Binadamu la Kizazi cha Kwanza baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Azimio hilo limeweka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu juu ya Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966.
Azimio hilo limeeleza kwamba kila binadamu yupo huru katika kushiriki na kuendesha nchi yake. Hivyo, uchaguzi unashirikisha Wananchi katika kuendesha nchi yao.
Makala hii itajikita kuzungumzia uchaguzi wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 hadi kipindi cha sasa.
UCHAGUZI MKUU BAADA YA MAPINDUZI YA 1964
Zanzibar, baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 haikuwa ikifanya uchaguzi hadi hapo katika miaka ya 1980.
Kwa wakati huo, nchi ilikuwa ikiendeshwa na Baraza la Mapinduzi na mamlaka ya kutunga Sheria yalikuwa kwa Baraza la Mapinduzi ambalo liliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Itakumbukwa kwamba mara baada ya Mapinduzi ya 1964, Serikali ilipitisha Sheria iliyojulikana; Sheria ya Uwezo wa Kutunga Sheria (Legislative Powers Law), ambayo kifungu cha 2 cha Sheria hiyo kilieleza kama ifuatavyo:
“The power to make law for the Government of the People’s Republic of Zanzibar is hereby vested in the President of the Republic acting by and with the advice and consent of Revolutionary Council”.
Ikimaanisha kwamba mamlaka ya kutunga sheria kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar itakuwa kwa Rais wa Jamhuri akifanya kazi kwa niaba na kushauriana na kupata ridhaa ya Baraza la Mapinduzi.
Hivyo, katika kipindi hicho, Baraza la Mapinduzi ndilo lililokuwa na mamlaka ya kutunga Sheria na wajumbe wa Baraza waliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Hali hiyo iliendelea hadi mwaka 1979 ambapo Serikali ilianzisha Katiba ya Zanzibar ya 1979 iliyoweka misingi ya haki za binadamu na demokrasia.
Katiba ilitoa uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa pamoja na haki ya kupiga kura. Katiba hiyo ilianzisha Tume ya Uchaguzi na ilipewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa Rais pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Serikali pia ilitunga Sheria ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar Namba 3 ya 1980. Sheria hii iliweka utaratibu na mchakato wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa kuwa kipindi hicho kilikuwa kipindi cha mpito, ambapo Serikali iliazimia kuimarisha demokrasia nchini, Katiba ya Zanzibar ya 1979 ilifutwa na kutaarishwa Katiba mpya ya Zanzibar 1984 na ilienda sambamba na kufutwa kwa Sheria ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar ya 1980 na kuanzishwa Sheria ya Uchaguzi namba 11 ya 1984.
Kwa kuwa idadi na mahitaji ya watu yanaongezeka, Serikali ililazimika kuimarisha kuweka mazingira bora yatakayokwenda sambamba na ongezeko na mahitaji ya watu.
Katika kuliendea hilo, Serikali ilifuta Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya 1984 na kutunga Sheria mpya ya Uchaguzi Namba 4 ya 2018.
Sheria hiyo mpya imetoa mamlaka kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kusimamia na kuratibu masuala yote ya Uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
Ifahamike kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni uchaguzi ulioendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984. Katiba hiyo imeweka ukomo wa uongozi wa Miaka Mitano kwa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
Mchakato wote unaratibiwa na Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya 2018 ambayo imeweka utaratibu wa kuendesha uchaguzi na kupiga kura.
Kama ilivyoelezwa kabla ya mwaka 1980 hakukuwa na uchaguzi. Uchaguzi, kuanzia mwaka 1980 hadi 1990, ulikuwa uchaguzi wa Chama kimoja cha siasa.
Baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha azimio la kuwa na vyama vyingi vya siasa 1992, uchaguzi tokea mwaka 1995 unaendeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi.
Kwa kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano inalazimika kufuata mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa.
Aidha, kifungu cha 5 cha Katiba ya Zanzibar, 1984 kimeeleza “Zanzibar itafuata mfumo wa Kidemokrasia wa Vyama Vingi vya Siasa wenye kuheshimu utawala wa sheria, haki za binaadamu, usawa, amani, haki na uadilifu”.
Hivyo, Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza kazi zake, inaratibu uchaguzi wa vyama vingi vya siasa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Usajili ya vyama vya Siasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni wa saba tokea Zanzibar ishiriki uchaguzi wa vyama vingi vya siasa kuanzia mwaka 1995.
NAMNA YA KUUNDA SERIKALI BAADA YA UCHAGUZI
Kama tunavyojua kwamba, Serikali za kidemokrasia zinajengwa na mihimili mikuu mitatu ya kuendesha Nchi.
Kifungu cha 5A cha Katiba ya Zanzibar, 1984 kimetambua mihimili hii kama ni mgawanyo wa madaraka wa kuendesha nchi ambayo ni mamlaka ya utendaji, mamlaka ya kutunga Sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Umma na mamlaka ya kutekeleza utoaji haki.
Katiba imefafanua kwamba mamlaka ya utendaji ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ni Baraza la Wawakilishi na mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ni Mahkama.
Katika mgawanyo huo, mamlaka mbili za kuendesha nchi ndizo mara zote zinaathiriwa moja kwa moja na Uchaguzi Mkuu. Nayo, ni ile mamlaka ya kiutendaji ambayo inahusiana na uchaguzi wa Rais na na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na mamlaka ya kutunga sheria ambayo inahusiana na uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Serikali za mitaa kwa upande wa uchaguzi wa madiwani.
Mamlaka ya utekelezaji wa utoaji haki, ni muhimili wa kipekee uliopewa kinga kwa muhimili wenyewe pamoja na watendaji wake kutoingiliwa katika kutekeleza majukumu ya utoaji haki.
Mara baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza mshindi wa kiti cha Urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi wa vyama vingi vya siasa, Rais mteule baada ya kula kiapo cha uaminifu anapaswa aunde Serikali.
Serikali anayopaswa kuiunda kwa mujibu wa Katiba ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama inavyofafanuliwa katika Kifungu cha 9(3): Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa katika umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.
Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa Zanzibar ulianza mwaka 2010 baada ya Serikali kupitisha Sheria ya Kura ya Maoni Namba 6 ya 2010.
Sheria ilitoa uhuru kwa Wananchi kupiga kura na kuamua muundo wa Serikali wanayoitaka na hatimaye kupata Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Muundo ambao baadhi ya nchi za Afrika kama vile Afrika ya Kusini wanautumia katika kuendesha nchi.
Sababu kuu ya kuanzisha kura ya maoni kwa Zanzibar ilikuwa ni kukabiliana na hali ya mpasuko wa kisiasa iliyokuwa ikiendelea katika visiwa vya vyetu vya Unguja na Pemba baada ya uchaguzi wa 1995 na 2000.
Ili kuondoa mpasuko huo, Serikali ilifanya maridhiano baina ya Chama ya Mapinduzi na Chama cha Wananchi Civic United Front (CUF). Maridhiano ya kwanza kutekelezwa yalishindwa na hatimaye muafaka wa pili ulifanyika. Muafaka huo ulipelekea kuanzisha Sheria ya Kura ya Maoni ya 2010 na baada ya Kura ya Maoni kukubalika ilipelekea kufanya Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ikiwemo Marekebisho ya Muundo wa Serikali.
Hivyo, ili kufuata masharti ya Katiba, baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika ni kuunda Serikali ambayo lazima iwe na Muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Mchanganuo wa Serikali hiyo umefafanuliwa katika Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Imekuwa ni utamaduni wa nchi nyingi za Jumuiya ya Madola, kabla ya kuunda Serikali Rais mara baada ya kuapishwa anamteua Mwanasheria Mkuu.
Umuhimu wa kumteua Mwanasheria Mkuu mwanzo ni kumuwezesha Rais kupata ushauri wa kisheria kabla hajatekeleza majukumu yake ikiwemo ya kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wakati kuunda Serikali.
Katika kuunda Serikali, kama ilivyoelezwa huko juu, Rais ataunda Serikali kwa mihimili miwili ambayo mihimili hiyo iliathiriwa moja kwa moja na uchaguzi.
Hivyo, kwa kuanzia, Rais atateua viongozi katika muhimili wa kiutendaji ikiwa ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.
Kwa mujibu kifungu cha 39 cha Katiba ya Zanzibar 1984, kimemtaka Rais ndani ya siku saba mara baada ya kushika madaraka, yaani baada ya kula kiapo, atamteua Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.
Kwa kuwa ilielezwa kuwa Muundo wa Serikali ni ya Umoja wa Kitaifa. Hivyo, Katiba imeweka sharti la mtu anaefaa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais lazima atoke kwenye Chama cha Upinzani kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais.
Iwapo chama kilichotokea nafasi ya pili kimepata chini ya asilimia kumi za kura zote za uchaguzi wa Rais au Rais hatokuwa na mpinzani, uteuzi wa Makamu wa Kwanza utafanywa kutoka chama cha upinzani kilichotokea nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
Aidha, Rais atamteua Makamu wa Pili wa Rais kutokana na miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Katika muendelezo wa kuunda Serikali Rais ataanzisha Wizara mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baada ya kuanzisha Wizara ndani ya siku kumi na nne baada ya kumteua Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais, atateua Mawaziri kwa kushauriana na Makamu wote wawili.
Mawaziri watateuliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Uteuzi wao utazingatia uwiano wa viti vya majimbo kwa vyama vya siasa vilivyomo ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Muundo wa Serikali pia utakuwa na Mapinduzi Baraza la ambalo linajumuisha Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na Mawaziri pamoja na wajumbe wengine ambao Rais ataona inafaa kuwateua.
Muundo wa Serikali unaweza kuwa na naibu mawaziri ingawa Katiba haijaweka ulazima wa uteuzi wa Naibu Mawaziri kama ulivyoweka ulazima kwa uteuzi wa Mawaziri na kutoa muda maalum kwa Rais kufanya uteuzi wao.
Uteuzi wa Naibu Mawaziri unafanywa na Rais kwa kushauriana na Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi ni Kiongozi muhimu sana katika muhimili wa kiutendaji na anashika nafasi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na kuwa Kiongozi wa Utumishi wa Umma kwa Zanzibar.
Rais baada ya kuunda Baraza la Mapinduzi atamteua Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambae atakuwa na dhamana ya Baraza la Mapinduzi, kupanga shughuli za mikutano na kuweka kumbukumbu za mikutano ya baraza na kufanya shughuli nyengine atakazopangiwa na Rais.
Katika kuhitimisha muundo wa Serikali kwa upande wa kiutendaji, Rais atawateua Makatibu Wakuu katika Afisi ya Rais, Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais na katika wizara mbalimbali kama Rais anakavyoona inafaa. Katiba ya Zanzibar haikuweka ulazima wa kuteuliwa naibu makatibu wakuu wa wizara.
Kwa upande wa muhimili wa kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma, Rais ni sehemu ya Baraza la Wawakilishi.
Kwa mujibu wa kifungu cha 63 cha Katiba kimeeleza Muundo wa Baraza la Wawakilishi utakuwa na sehemu mbili. Sehemu moja ni upande wa Rais na sehemu ya pili ni upande wa wawakilishi.
Katika sehemu ya Rais, Katiba imempa uwezo wa kuitisha Mkutano wa Baraza la Wawakilishi kama ni sharti la kuunda serikali mara baada ya uchaguzi.
Hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 90 na 91 cha Katiba ya Zanzibar, Mkutano wa Baraza la Wawakilishi utaitishwa si zaidi ya siku 90 baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi kupisha Uchaguzi Mkuu, Rais wa Zanzibar pekee amepewa uwezo wa kuitisha Baraza la Wawakilishi na kuendelea shughuli zake.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni mfumo wenye lengo la kupanua ushirikishwaji wa kuendesha nchi na kuwa na maamuzi ya pamoja baina ya vyama vingi vya siasa.
Mfumo huo umeleta maridhiano na manufaa katika jamii na kuonesha ukomavu wa demokrasia nchini.