Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar - AGCZ

Bendera ya Taifa
Ufahamu Ukomo wa Madai ya Kisheria
Elimu ya Sheria

Ufahamu Ukomo wa Madai ya Kisheria

04 Mar 2026 Na Safia Sultan-Wakili wa Serikali 123 views
Makala hii inatoa ufafanuzi wa ukomo wa madai ili kuhakikisha kwamba madai yanawasilishwa kwa wakati Mahkamani na kuweza kupatikana haki.

Ukomo wa madai ni moja ya misingi muhimu katika Sheria za Madai, ambapo dhana hii inaweka mipaka ya muda ambao ndani yake muhusika/mdai anapaswa kuwasilisha madai yake Mahkamani.

Lengo la kuwekwa kwa ukomo wa madai ni kuhakikisha kwamba madai yanawasilishwa kwa wakati Mahkamani ili kuweza kupatikana haki.

Pia kuona kwamba madai yanafikia mwisho maana milango ya madai haiwezi kufunguliwa milele.

Makala hii inatoa ufafanuzi wa ukomo wa ufunguaji wa kesi za madai.

Dhana ya ukomo wa madai

Dhana hii kwa Zanzibar inasimamiwa na Sheria ya Ukomo Sura ya 12 ya mwaka 1917 (Limitation Decree Cap 12 of 1917).

Ukomo wa madai kisheria ni muda maalum uliowekwa na sheria ambao ndani yake mtu anaweza kufungua kesi mahkamani kudai haki.

Muda huo maalum uliowekwa ukimalizika pasipokuwa na sababu zinazokubalika kisheria, mtu hawezi tena kufungua kesi na anazuilika kisheria kwa sababu muda wa kudai haki yake umemalizika (time barred).

Madai na ukomo wake

Kwa mujibu wa Sheria ya Ukomo Sura ya 12 ya mwaka 1917 (Limitation Decree Cap 12 of 1917), muda wa ukomo hutofautiana kulingana na aina za madai kwa mujibu wa Jadweli maalum lililopo katika Sheria hiyo.

Aina ya Dai Muda wa Ukomo
Migogoro ya Ardhi (Kurejeshewa ardhi) Miaka 12
Mikataba Iliyoandikwa na Kusajiliwa Miaka 6
Mikataba ya Kawaida/Deni la Pesa/Kodi Miaka 3
Uvunjaji wa Mkataba (Specific Performance) Miaka 3
Mishahara ya Wafanyakazi Mwaka 1
Kashfa (Libel/Slander) na Mashitaka ya Ovu Mwaka 1
Madai yenye msingi wa kisheria ya madhara Miaka 3
Jeraha la Mwili au Kufungwa Isivyo Halali Mwaka 1

Muda wa kipindi cha Ukomo wa Madai kuanza kuhesabiwa

Muda huanza kuhesabiwa pale tu sababu ya msingi ya kudai (cause of action) inapojitokeza. Kwa mfano, siku mkataba unapovunjwa au siku mtu anapovamiwa kwenye ardhi yake.

Kuhusu mazingira ya kusimama kwa muda, Sheria inatambua kuwa kuna nyakati mtu hawezi kufungua kesi. Muda unaweza kusitishwa ikiwa kuna:

Kizuizi cha Kisheria:

Mdai ni mtoto (chini ya miaka 18) au ana ugonjwa wa akili. Muda utaanza kuhesabiwa atakapofikisha umri wa utu uzima au kupata akili timamu;

Udanganyifu (fraud):

Ikiwa mdaiwa alificha ukweli au nyaraka kwa hila, muda UTAANZA kuhesabiwa pale mdai atakapogundua udanganyifu huo; au

Mdaiwa kuwa nje ya Nchi:

Muda ambao mdaiwa yuko nje ya Zanzibar hautahesabiwa katika kipindi cha ukomo.

Ukomo wa Madai katika migogoro ya ardhi, hapa ipo dhana ya Umiliki wa Kutwalia (Adverse Possession). Ikiwa mmiliki halali atakaa kimya kwa zaidi ya miaka 12 bila kuchukua hatua dhidi ya mvamizi aliyeendeleza eneo hilo, anaweza kupoteza haki ya kumtoa mvamizi huyo. Mahkama Kuu ya Zanzibar imewahi kusisitiza kuwa sheria hii haina "huruma" kwa yule anayechelewa kudai chake.

Katika kesi ya DAVID ANNOSIS IBONDE v. MSELEM SHAZIL AME (Represented by his recognised agent Khamis Ame Khamis). Mahkma Kuu ya Zanzibar, Kesi ya Rufaa Nam.6 ya 2021. Mhe. Abdul-hakim A. Issa, J alieleza kwa tafsiri isiyo rasmi “kwa kuzingatia masharti yaliyomo katika kifungu cha 4 mpaka 25 (vyote kwa pamoja),…

…..kila shauri litakalofunguliwa baada ya kupita muda wa ukomo uliowekwa kwa mujibu wa Jadweli husika litafutwa, hata kama suala la ukomo halijawekwa kama utetezi katika shauri hilo”, na shauri hili ilielezwa kwamba Mrufani/Mdaiwa alikuwa ni mvamizi wa ardhi lakini aliipata haki ya umiliki kwa kupita kwa muda wa miaka kumi na mbili (12).

Kwa ujumla, Sheria ya Ukomo wa madai ina nafasi muhimu katika mfumo wa haki kwa kuweka muda maalum wa kuanzisha madai Mahkamani kwani sheria inawasaidia wale wale walio macho na haki zao, na si wale wanaolala (Equity aids the vigilant, not the indolent).

Ukomo wa madai ni "upanga mkali" unaoweza kukata haki yako ikiwa hutaizingatia. Ni muhimu kwa kila mwananchi au mfanyabiashara kufuatilia madai yake mapema kabla muda haujapita (Time-Barred).

Ukishindwa kuzingatia muda huu, mahkama italazimika kuitupilia mbali kesi yako, hata kama una ushahidi wa wazi, kwani suala la ukomo ni la msingi kisheria.

Kuhusu Mwangaza wa Sheria

Mwangaza wa Sheria ni sehemu ya elimu kwa umma inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria, haki, wajibu na taratibu mbalimbali za kisheria.