Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Ndg. Shaaban Ramadhan Abdalla amesema Serikali kupitia Afisi ya Mwanasheria Mkuu inatumia gharama kutafuta wataalamu wa ndani na nje ya Zanzibar wa masuala ya Mikataba wanaoweza kutoa mafunzo kwa mawakili wa yatakayowasaidia serikali kuimarisha utendaji kazi zao.
Naibu Shaaban amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa mawakili wa Serikali yaliyohusu Misamaha ya Kodi katika Mikataba na kuongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza umahiri wa Mawakili katika kusimamia na kutekeleza mikataba kwa ufanisi.
Alisema, ana imani kuwa wataalamu hao watakidhi mahitaji na hivyo kusaidia kuongeza weledi kwa mawakili hao ili kulinda maslahi ya serikali na wananchi kwa ujumla.
Alisema malengo ya mafunzo hayo si tu kuwasaidia mawakili, bali kuisaidia nchi kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa, serikali ya awamu nane imejikitaka kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alibainisha kuwa nchi inahitaji kufaidika kwa kupata kodi kupitia mikataba ambayo serikali inaingia, hivyo ni vyema mawakili wakafahamu masuala ya kodi na misamaha yake ili watoe ushauri mzuri wakati wa kupitia mikataba hiyo.
Naibu Shaaban aliongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha taasisi zake na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa changamoto zinazojitokeza kushughulikia za katika kisheria sekta mbalimbali.
Akizungumza katika mafunzo hayo mkufunzi, Dkt. Michael J. Marere kutoka Taasisi ya Ushauri ya Loreme (LCG) alisema, kumekuwa na ombwe katika uandaaji wa mikataba na kwamba Serikali inaingia katika miradi mingi ya kimaendeleo ambapo pamoja na mambo mengine inahitaji kupata misamaha.
Dkt. Marere amesema, kazi iliyonayo Afisi ya Mwanasheria Mkuu ni kuhakikisha misamaha ya kodi inaendana na sheria hiyo na kwamba hilo ndio ombwe lenyewe.
Alisema ni jukumu la watendaji wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu kujua sheria za kodi hasa kwenye maeneo yanayohusu misamaha ya kodi ambayo haiendani na sheria.
Aliishauri Afisi kuendelea kutoa mafunzo mbali mbali kuhusiana na sheria za kodi hasa maeneo ya misamaha ikiwemo misamaha kwenye sheria za kodi za kimataifa ili Afisi hiyo iendelee kutoa ushauri unaozingatia maslahi ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Usimamizi wa Mikataba kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Ndg. Abeid Saleh, alieleza kuwa, mikataba ni nyenzo muhimu ya kisheria inayohitaji uangalizi wa karibu ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa maslahi ya taifa.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Uhusiano wa Kikanda na Kimataifa kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Ndg. Chai Ali Mohamed, alieleza kuwa, hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani itawasaidia wafanyakazi kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi katika kusimamia mikataba ya Serikali.
Wakati huo huo, Wakili wa Serikali Yakub Rajab aliishukuru Afisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo ya kuimarisha uwezo wao wa kitaalamu, hususan katika kipindi ambacho Zanzibar inashuhudia ongezeko la miradi mingi ya maendeleo na uwekezaji.
Habari
29 Jan 2026
44 views
Mawakili wa Serikali Wapigwa Msasa wa Kusimamia Mikataba
Muhtasari:
Mawakili wa Serikali wapatiwa mafunzo ya siku mbili kuhusu Misamaha ya Kodi katika Mikataba ili kuwaongezea ufanisi wa kazi zao.