Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA), imepata ushindi katika Maombi ya Madai Na. 10 ya Mwaka 2024.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Kesi na Mashauri ya Madai katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar, Said Salim Said alisema kesi hiyo ilifunguliwa na Saleh Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir dhidi ya Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar.
Said, ambaye ni Wakili wa serikali Mkuu, alisema katika maombi hayo, waombaji waliiomba Mahkama Kuu Zanzibar kupitia upya uamuzi wa Kamishna wa ZDCEA wa Aprili 22 mwaka 2024, uliotangaza kutaifishwa kwa mali mbali mbali zikijumuisha nyumba na viwanja vilivyopo maeneo tofauti ya Zanzibar, kwa madai kuwa mali hizo zilipatikana kutokana na mapato ya uhalifu.
Aidha Mkurugenzi Said alifahamisha kuwa katika maombi yao, waombaji walidai kuwa hatua ya kutaifisha mali hizo ilikuwa kinyume cha sheria kwa kuwa ilifanyika bila ya amri ya Mahkama.
Hata hivyo, alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahkama imebaini kuwa Kamishna alitumia mamlaka aliyopewa kisheria chini ya Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sheria Na. 8 ya Mwaka 2021.
Alifahamisha kuwa katika uamuzi alioutoa Juni 11 mwaka 2026, Mheshmiwa Jaji wa Mahkama Kuu H. S. Khamis (Tetere), alieleza kuwa waombaji hawakuweza kuthibitisha ukiukwaji wowote wa sheria au dosari za kiutaratibu ambazo zingehalalisha Mahkama kuingilia kati au kubatilisha uamuzi huo wa Kamishna.
Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa Mahkama iliridhika kuwa hoja za kisheria zilizowasilishwa na waombaj hazikuondoa wala kuathiri mamlaka ya Kamishna yaliyowekwa wazi na sheria husika.
Kutokana na sababu hizo, alisema Mahkama ilitupilia mbali maombi yote ya Waombaji na kuthibitisha uamuzi wa Kamishna wa Aprili 22 mwaka 2024 wa kutaifisha mali hizo kwa Serikali.
Uamuzi huo wa Mahkama ni miongoni mwa maamuzi ya mwanzo ya Mahkama Kuu ya Zanzibar, kuthibitisha na kuunga mkono mamlaka ya kisheria aliyopewa Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar ya kutaifisha mali zinazobainika kuwa zimetokana na mapato ya uhalifu, kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya Mwaka 2021.
Aidha uamuzi umekuja kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya na uhalifu wa kifedha, ili kuhakikisha kwamba mali zinazotokana na shughuli za uhalifu haziwanufaishi wahusika, bali zinarejeshwa kwa manufaa ya umma kwa mujibu wa Sheria.
Habari
18 Jun 2026
76 views
Serikali Yashinda Kesi Utaifishaji Mali Zilizohusisha Mapato ya Uhalifu
Muhtasari:
AGCZ na ZDCEA yapata ushindi katika Maombi ya Madai ya Na. 10 ya Mwaka 2024.