Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imeandaa mafunzo maalumu kuhusu mbinu za utafiti wa sheria kwa lengo la kuwajengea uwezo na umahiri watendaji wake katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa watendaji wa Idara ya Mapitio na Utafiti wa Sheria, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Dkt. Abdul-Nasser H. Hikmany, amesema mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwawezesha watendaji kufahamu kwa kina mbinu mbalimbali zinazotumika katika kufanya tafiti za kisheria.
“Kimsingi, mafunzo haya yamejikita katika mbinu za kufanya utafiti pamoja na namna sahihi ya kufanya marejeo ya kisheria, kutokana na umuhimu wake katika utekelezaji wa majukumu ya Idara yetu,” amefafanua Dkt. Hikmany.
Ameongeza kuwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu, kupitia Idara ya Utafiti na Mapitio ya Sheria, huandaa ripoti nyingi na za kina. Kutokana na hali hiyo, Afisi imeona umuhimu wa kuwajengea watendaji uwezo wa kutumia mbinu za kitaalamu katika kufanya tafiti na kuandaa ripoti.
Katika mafunzo hayo, watendaji wameelekezwa namna ya kupata vyanzo vya taarifa kupitia mitandao, maktaba na nyaraka mbalimbali. Pia wamefundishwa namna ya kuchambua taarifa, kufanya marejeo ya kisheria na kuandaa ripoti za utafiti kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Utafiti wa Sheria, Ndugu Yakub Rajab Juma, amesema mafunzo hayo yatawasaidia watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia weledi wa kitaalamu, kuanzia hatua ya awali ya utafiti hadi uandaaji wa ripoti ya mwisho.
“Tumefundishwa mbinu mbalimbali, zikiwemo namna ya kutafuta vyanzo vya taarifa pamoja na kuandaa ripoti zinazoendana na hadhi na viwango vya utafiti husika,” amesema Yakub.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Ndugu Rahma Salum Fundi, amesema mafunzo hayo yatawasaidia watendaji kuwa na mfumo mmoja wa uandaaji wa ripoti za kitafiti unaokidhi vigezo vya kitaalamu, ikiwemo matumizi ya mtindo unaofanana wa uandishi na marejeo.
Mafunzo hayo ya ndani kwa watendaji yalifanyika katika Ukumbi wa Mwanasheria Mkuu, Mazizini, Zanzibar. Mafunzo hayo pia yaliambatana na kazi mbalimbali za vitendo ili kuhakikisha kuwa washiriki wameelewa na wanaweza kutumia kwa usahihi maarifa waliyopatiwa.
Habari
28 Jul 2026
69 views
Mawakili Waongezewa Uwezo katika Utendaji Kazi wao
Muhtasari:
Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imetoa mafunzo ya mbinu za utafiti wa sheria kwa watendaji wake ili kuwaongezea maarifa na kuwajengea uwezo wa kufanya tafiti, kupata vyanzo vya taarifa na kuandaa ripoti za kitaalamu kwa lengo la kuimarisha utendaji wa kazi.