Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji, amewataka Mawakili wa Serikali kuwa na uelewa wa sheria za kimataifa, mikataba ya kifedha na mbinu za majadiliano wakati wa kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mikataba ya mikopo ili kulinda maslahi ya Taifa.
Dkt. Mwinyi ametoa wito huo huko katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Mwanasheria Mkuu, Ndg. Shaaban Ramadhan Abdalla kwenye ufunguzi wa mafunzo yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Madinat el Bahr.
Alisema tofauti na mikopo ya masharti nafuu, mikopo ya kibiashara huja na vigezo na viwango vya kibiashara vinavyoendana na soko, masharti ya ulipaji yenye ukomo na uwajibikaji mkubwa na mara nyingi huambatana na masharti ya kisheria yenye uzito mkubwa.
Alitahadharisha kuwa, mikopo hiyo huhitaji umakini wa hali ya juu katika maandalizi, majadiliano na utekelezaji wake. “Lengo ni kuhakikisha kuwa Serikali haiingii katika mikataba itakayosababisha kudumaza uchumi wa nchi kwa muda mrefu”, alisema Dkt. Mwinyi.
Alibainisha katika awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuna ongezeko la mahitaji ya rasilimali za kifedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, bandari, viwanja vya ndege na vituo vya afya.
Alisema ili kukabiliana na mahitaji ya kifedha, Serikali imekuwa ikitumia mbinu za upatikanaji wa fedha, ikiwemo utaratibu wa kupata mikopo ya kibiashara.
Alieleza kuwa mikataba ya aina hiyo mara nyingi huandaliwa kwa kufuata viwango vya kimataifa na hujumuisha vipengele muhimu ikiwemo sheria itakayotumika, utaratibu wa utatuzi wa migogoro hususan kupitia usuluhishi wa kimataifa, dhamana za Serikali na mgawanyo wa hatari kati ya wahusika wa mkataba.
“Kutokana na upekee huo, ni dhahiri kwamba mawakili wa Serikali wanapaswa kuwa na uelewa mpana wa sheria za kimataifa, mikataba ya kifedha, pamoja na mbinu za majadiliano kwa ajili ya kulinda maslahi ya taifa katika mikataba hii”, alisema Dkt. Mwinyi.
Alisisitiza kuwa, utaratibiwa kupata mikopo unahusisha mikataba mikubwa baina ya Serikali na wakopeshaji.
Hali hiyo inaweka wajibu mkubwa kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na mawakili wa Serikali kwa ujumla, kuhakikisha mikataba yote inafanyiwa uchambuzi wa kina wa kisheria kabla ya kutiwa saini kwa ajili ya utekelezaji wake.
Kadhalika, alisema mawakili wa Serikali wanatakiwa maslahi kuhakikisha ya Serikali yanalindwa kikamilifu, kuhakikisha kuwa masharti ya mikataba ni ya haki, wazi na yanayotekelezeka na hatari zote zinazoweza kujitokeza zinatambuliwa mapema na kudhibitiwa ipasavyo.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Sheria kutoka CRDB, Pascal Mihayo, alisema wamekuwa wakifanya miradi mikubwa kwa ushirikino na serikali kufanikisha mikopo hiyo.
“Tumekuwa tukifanya mikopo hii na Serikali chini ya Mwanasheria Mkuu, lakini kutokana na uzoefu wa muda mrefu, kwa hiyo tumeona ni vyema kuweka mafunzo na majadiliano namna tunavyoweza kusaidiana katika kuingia mikataba”, alisema Mihayo.
Alieleza katika mafunzo hayo wameangalia mambo muhimu ya kufanyika kabla, wakati na baada ya kuingia mikataba ili kukwepa mitego inayoweza kuhatarisha maslahi ya umma katika mikataba hiyo.
Alisema awali mikataba ilikuwa inaweza kuchukua hadi miezi sita mpaka kukamilika lakini baada ya mafunzo hayo wanatarajia itafupishwa muda ili Serikali ipate fedha haraka kwa ajili ya maendeleo.
Alieleza kuwa mikataba ambayo ni dhaifu Serikali inaweza kupata hasara kwani umuhimu wa mkataba ni kuuangalia kabla ya kuingia kwani inatakiwa kuhakikisha wanalinda maslahi yao.
Naye, Meneja wa CRDB Tawi la Zanzibar, Fatma Nassor alisema watafungua fursa nyingi kwani mambo ya sheria yakiwa sawa hata biashara zao zitazidi kuimarika.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Rasilimali Watu, Utawala na Mipango kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Dkt. Abdul-Nasser H. Hikmany alisema katika awamu hii ya nane, Serikali imekuwa ikiingia katika mikataba inayochochea maendeleo, hivyo mafunzo hayo yatawajengea uelewa mkubwa ili kusaidia kuitolea ushauri mikataba inayokuja katika Afisi yao.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Ushauri, Ndg. Latifa Suleiman, alisema kabla ya kuingiwa kwa mikataba, kuna haja ya wanasheria kuifahamu vyema mikataba hiyo kila kipengele ili wasaidie kutoa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kuifanya mikataba hiyo kuwa na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Habari
20 Apr 2026
62 views
Mawakili Watakiwa Kujiongeza Kitaaluma Kwenye Mikataba, Sheria za Kimataifa
Muhtasari:
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji, amewataka Mawakili wa Serikali kuwa na uelewa wa sheria za kimataifa, mikataba ya kifedha na mbinu za majadiliano wakati wa kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mikataba ya mikopo ili kulinda maslahi ya Taifa.