Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua za kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi kwa Muhimili wa Mahkama ili kuzidisha uwajibikaji wa upatikanaji wa haki nchini.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipomuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria Zanzibar, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Wete kisiwani Pemba.

Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imewekeza zaidi shilingi Bilioni 13.6 kwa ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahkama ambayo yanaendana na uwekaji wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi.

Aidha, Mhe. Hemed alifahamisha kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika matumizi ya TEHAMA kuelekea Serikali Mtandao, ili kutimiza azma ya kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali hasa katika matumizi ya mfumo wa usimamizi wa mashauri na mifumo itakayozidisha mchakato mzima wa upatikanaji wa haki.

Alisema kupitia mfumo huo usajili wa mashauri utakuwa rafiki, usikilizaji na uamuzi wa mashauri utafanyika kwa haraka sambamba na upatikanaji sahihi wa takwimu, kuongezeka kwa uwazi na kukuza uwajibikaji miongoni mwa wadau wa Sheria.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya maadhimisho hayo, isemayo “Maboresho ya Mfumo wa TEHAMA kwa Taasisi za Sheria” alisema Afisi ya Mwanasheria Mkuu imenunua vifaa vya mfumo wa kieletroniki kwa lengo la kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Afisi hiyo.

Alisema, kwa sasa Afisi ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mshauri Elekezi atakayesimamia uandaaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu na kusimamia hatua muhimu za utekelezaji wa majukumu ya Afisi.

Dkt. Mwinyi alifahamisha kuwa, kwa hatua ya awali, mfumo huo utahusisha taarifa muhimu za Mawakili wa Serikali wanaofanya kazi au wanaosimamiwa na Afisi ya Mwanasheria Mkuu, pamoja na kuweka kumbukumbu za hatua mbali mbali zinazopitiwa katika mikataba ya Serikali na kazi nyengine zinazofanywa na Afisi.

Katika hatua za kujiwekea taratibu za kazi zinazoeleweka na kutekelezeka kwa umakini na ufanisi, Afisi ya Mwanasheria Mkuu imeandaa Miongozo ya Kiutendaji (Manuals) na tayari Afisi imechapisha na kusambaza Muongozo wa Uandishi wa Sheria ambao unatoa maelezo na utaratibu mzima wa uandishi wa sheria na kanuni nchini.

Akitoa salamu za Mahkama, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla alisema Matumizi ya TEHAMA yataleta mageuzi makubwa ya kiutendaji kwa kufanya kazi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika kufikia upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Jaji Khamis alisema mifumo mitano imeundwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wa mahkama ikiwemo mfumo wa usimamizi wa mashauri ambao utazifanya mahkama kuondokana na matumizi ya karatasi na mawakili watafungua mashauri ya kesi bila ya kufika mahakamani.

Jaji huyo aliitaja mifumo inayotumiwa na Mahkama za Zanzibar kuwa ni pamoja na mfumo wa usimamizi wa mashauri, Mfumo wa ZAN-WAKILI, Mfumo wa Tume ya Utumishi ya Mahkama, Mfumo wa Malalamiko na utoaji wa maoni pamoja na Mfumo wa Uhifadhi wa hukumu za Mahkama.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Mwalim Dkt. Haroun Ali Suleiman amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na watendaji wa Mahkama katika kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora, wezeshi na salama hasa kutokana na umuhimu wa utendaji kazi wa Muhimili huo.