Wananchi wa Shehia ya Vitongoji na Kibokoni Kisiwani Pemba wameishukuru Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa kuwapa elimu ya kisheria, kwani hawakuwa na ufahamu wa kutosha wa mambo mambalimbali ya kisheria.

Wakizungumza hayo wakati Mawakili wa Afisi hiyo walipokwenda kutoa elimu kwa wananchi hao, ambapo walisema Afisi hiyo imewafikia katika wakati muafaka hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawajui kutofautisha kati ya makosa ya jinai na mashauri ya madai.

Sheha wa Shehia ya Vitongoji, Bw. Salim Ayoub Suleiman alisema, “Wengi wetu hatujui kutofautisha makosa ndio maana watu anaingia katika hatia kwa kukosa tu uelewa wa sheria”.

Miongoni mwa mambo waliyolalamikia kutokuwa na uelewa ni pamoja na taratibu za ukamataji wa Polisi kwa watuhumiwa na sheria ya udhalilishaji waliyodai inawatia wanaume wengi hatiani kuliko wanawake.

Aidha walilalamikia Mahkama ya Ardhi kwa kudai kuwa inawapa wasiwasi wa kupata haki wanyonge pale wanapokuwa na kesi za migogoro ya ardhi dhidi ya watu wenye uwezo.

Mzee Omar Mjaka, mkaazi wa Vitongoji aliwashukuru Mawakili hao kwa kufika katika Shehia yao na kufahamu hali halisi ya matatizo yanayowakabili ikiwemo migogoro ya ardhi, mazingira na maamuzi ya kimahkama ambayo alidai hayawafurahishi.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha mada kuhusu migogoro ya ardhi, Mratibu wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu Pemba, Ndg. Massoud Nassor Mohammed, alisema migogoro hiyo ya ardhi imekithiri katika maeneo mbalimbali kutokana rasilimali hiyo kupanda thamani.

Mbali na hilo, aliwaomba wananchi hao pale wanapowaazima wenzao mashamba kwa ajili ya kilimo, wasiwaruhusu kupanda miti ya kudumu ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Ndg. Safia Sultan akiwasilisha mada ya ukomo wa madai, alisema migogoro ipo mingi katika jamii hivyo kuna haja ya kujua taratibu za kufungua ashauri ya madai ili kupata haki.

“Kesi zote za madai zinazo muda wake maalum wa kuzifungua Mahkamani, hivyo watu wasibweteke kufungua kesi muda wanaotaka wao, ni kosa na kunaweza kumkosesha mtu haki zake”, alisema Wakili huyo.

Akitoa mfano wa sheria ya ukomo wa masuala ya madai, alieleza kuwa, ukomo wa mtu kufungua dai mahkamani ni miaka 12 na ikitokea mtu kufungua dai baada ya miaka 12, dai hilo ni batili kwani sheria ya ukomo inamzuia.

Aidha alieleza kuwa madai mengine kama ya Pesa, kusababishiana madhara, kubadilisha matumizi ya bidhaa au vifaa, kuvunja mkataba na madai ya mishahara, yote yana ukomo maalum wa muda. Hivyo, amesisitiza jamii kupata elimu.

Kuhusu suala mabadiliko Wakili Jecha Vuai, alisema hilo ni suala mtambuka ambalo litahitaji kuzungumzwa pale watu wanapokutana kutokana na umuhimu wake.

Aidha Wakili Jecha aliwaomba wananchi kisiwani Pemba kufika Afisi ya Mwanasheria Mkuu huko Chake Chake kwa lengo la kujifunza sheria ili kujua haki na wajibu wao.

Afisi ya Mwanasheria Mkuu miongoni mwa majukumu yake ni kutoa elimu kwa jamii ambapo imejipangia utaratibu wa kufika katika shehia za mijini na vijijini kwa lengo la kuwajengea wananchi uwezo wa kisheria ili kuwasaidia kuepuka kuingia katika makosa ya kisheria.