Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Ndg. Sultan Said Suleiman, amewahimiza wafanyakazi wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kununua nyumba za kisasa zinazojengwa na Shirika hilo kupitia mfumo wa bei nafuu (PSHS) unaolenga kuwawezesha wananchi na watumishi wa umma kumiliki makazi bora.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa mpango wa kuwamilikisha watumishi wa umma nyumba kupitia mfumo wa Public Service Housing Scheme (PSHS) pamoja na utaratibu wa Zero Interest, Ndg. Sultan amesema mpango huo unatoa unafuu wa malipo kwa njia ya makato madogo ya mshahara kwa kipindi kisichopungua miaka 25, hivyo kuongeza uwezo wa watumishi wengi kumudu gharama za nyumba hizo.
Ameeleza kuwa lengo la mipango hiyo si tu kuwapatia wananchi makazi ya kisasa na salama, bali pia kuchangia uboreshaji wa mandhari ya miji ya Zanzibar ili iendane na kasi ya maendeleo ya kisasa.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo zinaendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inayolenga kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii ikiwemo barabara, masoko, hospitali na viwanja vya michezo.
Aidha, Ndg. Sultan amewaomba wanasheria wa serikali kushiriki kikamilifu katika kuandaa na kufanya marekebisho ya sheria zitakazosaidia kudhibiti ujenzi holela, hususan katika maeneo ya mijini.
Kwa upande wao, wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wamepongeza juhudi za Shirika la Nyumba Zanzibar katika kuendeleza miradi ya makazi ya kisasa, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kubadili mitazamo na matarajio yao kuhusu kumiliki nyumba bora.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mapitio ya Sheria na Utafiti kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Dkt. Abdul-Nasser Hikmany, ameipongeza Serikali kwa ubunifu huo unaotekelezwa kupitia ZHC, akisema ni suluhisho madhubuti kwa changamoto ya makazi inayowakabili wananchi wengi wa Zanzibar.
Ameeleza kuwa wananchi wengi hulazimika kutumia gharama kubwa na muda mrefu kujenga nyumba zisizo na viwango hivyo, utaratibu huo utawawezesha wafanyakazi na wananchi wengi kumiliki nyumba za kisasa kwa haraka.
Awali, maafisa wa masoko na milki wa Shirika la Nyumba Zanzibar waliwasilisha taarifa ya miradi mbalimbali ya nyumba za kisasa pamoja na mifumo wezeshi ya uuzaji, ikiwemo miradi ya Kisakasaka (B na D).
Habari
14 Apr 2026
32 views
Watumishi wa Umma Wahimizwa Kuchangamkia Fursa za Nyumba za Kisasa
Muhtasari:
Watumishi wa Umma Wahimizwa Kuchangamkia Fursa za ununuzi wa Nyumba za Kisasa Kupitia Mpango wa PSHS.