Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji amewanasihi waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kutenda mema zaidi baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kuthibitisha uchamungu wao.

Ametoa nasaha hizo katika hafla ya Futari iliyoandaliwa na afisi yake na kuwajumuisha wananchi mbali mbali ikiwemo watoto yatima huko Mazizini, Zanzibar.

Amesema haipendezi kutenda matendo mema katika kipindi cha Ramadhani peke yake na kupunguza kufanya matendo hayo miezi mingine kwani kwa kufanya hivyo lengo la uchamungu itakuwa halijafikiwa.

“Ni vyema ibada tunazozinafanya katika Mwezi huu kama vile kusoma Quran, kutoa sadaka na visimamo vya swala za usiku tunapaswa kuziendeleza katika miezi mingine” alinasihi Mhe. Mwanasheria Mkuu.

Aidha, amewashukuru wote walioungana naye katika hafla ya Futari hiyo, huku akisisitiza ushirikiano kwa jamii ni nguzo muhimu katika kuimarisha umoja wa Waumini na Wananchi kwa ujumla hususan katika kipindi cha Ramadhani.

Ameongeza kuwa, ushiriki wa viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, na wananchi kwa ujumla katika Futari hiyo ni ishara ya mshikamano wa kijamii na kiroho.

Mwanasheria huyo amekumbusha haja ya kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili wapate wepesi na utulivu katika majukumu yao ya kiuongozi.

Aidha amewapongeza walezi wa watoto yatima kwa jukumu zito la kuwalea watoto hao katika maadili mema na kuwaomba waendelee kuwa na subra katika malezi yao.

“Kwa hakika watoto yatima tunatakiwa kuwa nao pamoja katika nyumba zetu na tusiishie tu kula nao mara moja kwa mwaka kama wengi wetu tunavyofanya” amesema Dkt. Mwinyi.

Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Shaaban R. Abdalla amewashukuru wote waliotoa mchango wao wa hali na mali kufanikisha hafla hiyo, akiwataka waendelee kudumisha mshikamano na ushirikiano katika kipindi chote cha Ramadhani na baada ya mwezi mtukufu kumalizika.

Akitoa nasaha katika shughuli hiyo Mjumbe wa Baraza la Maulamaa Zanzibar, Shekh Saleh Battash amesema ni muhimu kuziendeleza hafla kama hizo, kwa kuwa husaidia kukuza maelewano, upendo na ushirikiano baina ya wananchi wa Zanzibar.

Mkuu wa Divisheni ya Fatwa kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shekh Ali Muombwa amesema ipo haja kwa Waumini kuyaendeleza mazuri yote waliyokuwa wanayafanya katika kipindi cha Ramadhani ili waendelee kuwa waja wema muda wote.

Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imejiwekea utaratibu kwa Wafanyakazi wake kufutari pamoja kila ifikapo Mwezi wa Ramadhani, shughuli ambayo huwashirikisha watu mbalimbali wakiwemo watoto yatima.